Social Icons

Alhamisi, 5 Juni 2014

FUGENI NYUKI KUONDOKANA NA UMASIKINI‏



Na Samwel Mwanga-Maswa
 
WANANCHI  wameshauriwa kufuga nyuki ili waweze kujiongezea kipato na
kuwainua kiuchumi na hivyo kuondokana na umasikini kwa kuwa ufugaji
huo ni moja ya shughuli za maendeleo.
 
Ushauri huo umetolewa  jana na Ofisa Ufuatiliaji na Tathimini wa Mradi
wa Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira ya Ziwa Victoria(LIVEMPII),Paul
Kariuki mara baada ya kutembelea Mradi wa Ufugaji nyuki katika kijiji
cha Ipililo wilayani Maswa mkoani Simiyu.
 
Alisema kuwa fursa hiyo waliyoipata ni nzuri na hivyo ni vizuri
wakaitumia kwa uzalishaji kuliko kutegemea kila kitu watafanyiwa na
serikali ili waweze kuondokana na umasikini kwa wananchi hasa waishiyo
maeneo ya vijijini.
 
“Umasikini sasa basi ndugu zangu wananchi hasa wa hapa Ipililo mseme
kuwa umasikini mmeanza kuuaga kuanzia hapa kutokana na ufugaji wa
nyuki ambao unafaida kubwa kwani tunaweza kupata asali pamoja na Nta
ambazo  zina bei kubwa kulingana na mahitaji yake ”alisema.
 
Kariuki ambaye aliambatana na wakulima na wataalam mbalimbali wa
mazingira kutoka nchini Kenya waliokuwa katika ziara ya siku tatu
wilayani Maswa kutembelea Miradi ya LIVEMP II Wilayani humo alisema
kuwa wafugaji nyuki pia husaidia kuhifadhi mazingira.
 
 “Ufugaji wa nyuki huhifadhi mazingira kwani kwa kutundika mizinga ya
nyuki  kwenye misitu  wanakijiji  wanashindwa  kuvamia misitu hiyo na
wale wavamizi wakorofi wanaovamia misitu hiyo hukabiliana na nyuki kwa
kuumwa”alisema.
 
Awali akisoma taarifa ya Mradi huo unaofadhiliwa na LIVEMP II,Ofisa
Kilimo wa Kata ya Ipililo,Inocent Kavela alisema kuwa kutokana na
mizinga waliyonayo 185 iliyotundikwa wanatarajia kuvuna kiasi cha kilo
2500 za asali na Nta kilo 278.
 
‘Matarajio ya uvunaji wa mazao ya nyuki tunategemea kuvuna kiasi cha
Kilo 2500 na Nta kilo 278 na katika soko la sasa bei ya kilo moja ya
Sali ni shilingi 10,000/= hadi 12,000/= na Nta ni shilingi 15,000/=
hadi 25,000/= kwa kilo”Alisema.
 
Mradi wa ufugaji wa nyuki katika kijiji cha Ipililo unawahusisha
wanakikundi wapatao 27 kati yao wamawake 11 na wanaume 16 na kiasi cha
Shilingi 30,914,600/= zimetolewa na LIVEMP II kuutekeleza kwa kipindi
cha Mwaka 2013/2014.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni