Mlele, Katavi
Wizara
ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu
imewezesha kila mkoa nchini kutundika mizinga 50 katika kuazimisha Siku
ya Kutundika Mizinga kitaifa iliyofanyika Machi 18, Mwaka huu.
Akizungumza
wilayani hapa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. M.K
Tarishi alisema siku hii inaadhimishwa kitaifa katika Msitu wa Mlele
Wilaya ya Mlele na mikoa yote Tanzania Bara inaadhimisha katika ngazi ya
Mkoa kwa kutundika jumla ya mizinga 1,400 katika sehemu mbalimbali za
mikoa husika.
Aliongeza
kuwa Mizinga hiyo imekabidhiwa kwa vikundi vya ufugaji nyuki ili iwe ni
chachu ya kuendeleza ufugaji Nyuki kwa kutumia mbinu bora za ufugaji
Nyuki unaolenga kumfanya mfugaji aweze kufuga kibiashara ambapo
atatakiwa kuwa na mizinga yenye makundi ya Nyuki isiyopungua 30 ambayo
ndiyo yenye tija kibiashara.
Alisisitiza
kuwa ufugaji wa kibiashara unamfanya mfugaji aweze kuzalisha kiasi cha
kilo 450 kwa msimu chenye thamani ya Tshs. 1,500,000 na nta kilo 30
ambazo zina thamani ya Tshs. 150,000 ambayo ni mara mbili na nusu kwa
wastani wa pato la mtazania.
Tathimini
ya Siku ya Kutundika Mizinga mwaka jana inaonesha kuongezeka mwitikio
wa jamii katika Ufugaji Nyuki. Uzalishaji wa asali umeongezeka kutoka
tani 9,800 za asali na nta tani 625 kwa mwaka 2012/2013 hadi tani 19,000
za asali na tani 1,200 za nta kwa mwaka 2013/2014.
“Thamani
ya kiasi hicho cha uzalishaji katika ngazi ya mfugaji ni sawa na
billion 66.5. Lengo ni kuongeza uzalishaji kwa asilimia 50 kwa mwaka
katika kipindi cha miaka mitano ijayo,” Alisema Bi. Tarishi.
Wakati
huo huo, Wakala wa Huduma za Misitu imeanzisha mkakati wa uzalishaji wa
makundi kwa kutumia uzalishaji wa malkia ili kuhakikisha mizinga
inakuwa na Nyuki badala ya kusubiria makundi yaingie yenyewe kwenye
mzinga.
Akielezea
kuhusu Mkakati huo, Bi. Tarishi alisema Mafunzo ya uzalishaji wa malkia
na usimamzi wa makundi ya nyuki yalianza tokea mwaka 2013
yakishirikisha wataalamu 47 kutoka Kanda saba za Wakala na wafugaji
nyuki 10 ambao walifanya mafunzo hayo kwa vitendo.
Alisema
jumla ya malkia 120 wamezalishwa kwa kipindi cha miaka miwili cha
mafunzo kwa lengo la kusambaza elimu hiyo ya uzalishaji wa malkia
nchini.
Hata
hivyo, alisema pamoja na ongezeko hilo uzalishaji bado ni mdogo (14%)
ukilinganisha na uwezo wa nchi yetu wa kuzalisha tani 138,000 za asali
na tani 9,200 za nta kwa mwaka.
Aliongeza
kuwa katika kuboresha tasnia ya ufugaji nyuki ni kuwawezesha wafugaji
kuwa na umoja wao ili kurahisisha huduma za ughani, kukabiliana na
changamoto za masoko na kudhibiti ubora wa mazao ya nyuki.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dkt Rajabu Rutengwe alisema mkoa
wake utahakikisha katika kila halmashauri ya mkoa kunakuwa na kituo cha
kukusanyia asali ili kuweza kuthibiti ubora wa asali kwa kupima asali
hiyo.
“Nimeshaagiza
kila halamashauri kuhakikisha imetenga bajeti ya kuanzisha kituo cha
kukusanyia asali ili kuweza kupata asali bora na uhakika wa soko kwa
wafugaji nyuki, utekelezaji wa suala hili utaanza mara moja katika mwaka
ujao wa fedha katika kuhakikisha wananchi wa Katavi wanajiongezea
kipato, lishe, dawa na kuhifadhi mazingira,” alisema Dkt. Rutengwe.
Kaulimbiu
ya siku ya taifa ya kutundika mizinga mwaka huu ni ilikuwa “BORESHA
UFUGAJI NYUKI LINDA UBORA WA MAZAO YAKE”. Kauli mbiu iliyoenda pamoja na
MKUKUTA II unaosisitiza kuondoa umasikini kwa wananchi na kuchangia
katika pato la Taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni